Thursday 24 October 2013

NIMEAMINI, KWELI DUNIA MSONGAMANO!

Marehemu Freddie Ndala Kasheba enzi za uhai wake
NDUGU zangu, napenda kuwakaribisha katika makala za aina hii zihusuzo muziki. Hapa tutakuwa tukizisawiri nyimbo mbalimbali zenye ujumbe maridhawa kwa maisha yetu. Leo hii niemamua kuanza na kibao hiki cha al-marhum Supreme Freddie Ndala Kasheba kisemacho ‘Dunia Msongamano’, ambacho alikiimba na bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS) mwanzoni mwa miaka ya 1980 (mwaka 1982).
Hakuna shaka kwamba pamoja na kuimbwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini mashairi yake yamebeba ujumbe murua unaohusu maisha yetu ya sasa na hata yajayo. Siyo ajabu kinapopigwa – aua hata ninapowakumbusha hapa – baadhi yenu mnalinganisha na mambo yaliyowatokea ninyi wenyewe ama ndugu na jamaa zenu.
Ndugu zangu, maradhi humpata mtu yeyote yule, na kwa hakika kuugua siyo kufa! Kama ambavyo mti humea wakati wa masika na kupukutika wakati wa kiangazi, ndivyo ilivyo miili ya binadamu. Wakati mwingine kupata maradhi ndiko kuukomaza mwili.
Lakini inashangaza baadhi ya walimwengu, tena wakati mwingine wale ambao ni watu wa karibu yetu kabisa, hutokea kuombea kwamba fulani afe. Wengi hugeuka watabiri kila wanaposikia fulani anaumwa, na moja kwa moja mawazo yao huwapelekea kuamini kwamba watu hao hawatapona, bali watakufa!
Walimwengu ni watu wa ajabu kabisa ndugu zangu. Pindi wanapomuona fulani anasumbuliwa na maradhi, wao tayari huanza kupiga hesabu ya lini atakufa na wapi atazikwa!
Watu wa aina hii ni wengi sana ndani ya jamii yetu na inaonekana wamepitiwa hata na maneno ya wimbo wa Salamu kwa wagonjwa ulioimbwa na Omar Kungubaya miaka ile ya 1970 yasemayo; “…Ajuaye Bwana Mungu kwa mzima kuwa mfu, mgonjwa kuwa salama…”
Binafsi naamini kwamba kila nafsi itaonja mauti, kwa sababu sisi sote ni mavumbi na mavumbini hatuna budi kurejea. Hivyo, suala la kufa huwa silihofii kabisa, ninachokihofia ni kwamba nitakuwa katika kundi gani baada ya kufa. Daima wenye hekima humuomba Mungu awaongoze katika haki na kuwaombea wengine washike mwenendo mwema, si ndivyo jamani?
Kasheba hakukosea alipokitunga kibao hiki na kukiimba akiwa na Orchestra Safari Sound ‘wana-Dukuduku’ kisemacho Kwamba kilikuwa ni kisa cha kweli kilichomtokea mwenyewe hilo haliwezi kuondoa ukweli kwamba mambo haya yanatokea ndani ya jamii zetu. “…Mawazo yamenijia leo, Ya Mzee wangu alokuwa akisema, Dunia ni msongamano wa watu wenye akili tofauti, Ukitaka kuishi vema lazima uwe na utulivu, Ukitaka kuishi vema fikiri kabla ya kujibu, Jifunze kwa walimwengu, na walimwengu wajifunze kwako, Dunia ni kuona mambo, Na halafu kuyasahau…”
Ni kweli kabisa, dunia ni msongamano kwa sababu imejaa watu wengi wenye mawazo tofauti, ambao wanadhani kwamba mtu akiugua basi atakufa tu, tena yawezekana kabisa wakawa wamempangia siku, saa na namna kifo chake kitakavyokuwa.
Watu wa aina hii tunawashuhudia jamani, hawaendi kuwaona wagonjwa mpaka kwanza waulizie; “Anaumwa nini?” “Vipi amekonda?” “Sijui kama atapona, hivi umeomuona alivyo?” Basi hukumu hizi na nyingine nyingi ndizo hutawala mawazo ya watu hawa, na hata pale wanapokuwa wanakwenda kuwatazama wagonjwa huwa ni kama maigizo fulani tu kwao, yaani kana kwamba wamekwenda kuthibitisha hisia zao kwamba watu hao hawatapona! Utadhani wao ni maswahiba wa Mungu na wanajua mipango yake!
Kweli naamini maneno ya Kasheba; “…Dunia msongamano, Kasema baba, Nimeyaona leo nakubali mie, Wengine hupendelea kufurahia, Wanaposikia fulani kafa…” Lakini wanasahau kwamba; “… Kufa kwa binadamu hupangwa na Mungu, Namuomba Mwenye Enzi anipe maisha eeh.”
Ndiyo, wanasahau kwamba maradhi yawapatayo wanadamu wakati mwingi si ya mauti, bali hutokea ili Mungu aweze kutukuzwa kwayo. Lakini bila kupatwa na masahibu pengine huwezi kamwe kuitambua tabia ya upande wa pili ya ndugu na jamaa zetu.
Ninachoweza kusema ni kwamba, tuwaombee kwa Mungu awasamehe wale wote wenye tabia ya kupenda kuwatabiria wenzi wao kwamba watakufa. Wale wenye tabia ya kujifanya madaktari bingwa wa kupima watu kwa macho! Wale wenye kawaida ya kujifanya miungu wa dunia kwa kuweza kutoa hukumu wakati wakijua kwamba hakimu pekee ni Mungu!
Hebu burudikeni na kibao hiki, lakini kusema kweli nahitaji sana mchango wenu katika mada hii.

AAhhhh DUNIA MSONGAMANO
Mawazo yamenijia leo,
Ya Mzee wangu alokuwa akisema,
Dunia ni msongamano wa watu wenye akili tofauti,
Ukitaka kuishi vema lazima uwe na utulivu,
Ukitaka kuishi vema fikiri kabla ya kujibu,
Jifunze kwa walimwengu, na walimwengu wajifunze kwako,
Dunia ni kuona mambo,
Na halafu kuyasahau

Kibwagizo:
Dunia msongamano,
Kasema baba,
Nimeyaona leo nakubali mie,
Wengine hupendelea kufurahia,
Wanaposiikia fulani kafa,
Kufa kwa binadamu hupangwa na Mungu,
Namuomba Mwenye Enzi anipe maisha eeh

Ndugu yenu,

Daniel Mbega

Mnaweza kunitumia mchango wenu kwa sms ama kunipigia kupitia kilongalonga – 0715 – 070 109, au barua-pepe: brotherdanny5@gmail.com.

No comments:

Post a Comment