Thursday 24 October 2013

WEWE MTOTO ROSA HEBU NENDA SHULE

Marijani Rajabu Marijani 'Jabali la Muziki'

Na Daniel Mbega

AHLANI Wasaalani mabibi na mabwana ambao mnaperuzi ukurasa huu na blog hii ambamo tunabarizi na kujikumbusha ile mikito ya zamani, miziki ya Bakulutu ambayo mpaka leo bado ni keki kweli inapodundwa.
Siku moja nikiwa kwenye daladala, ule usafiri wetu akina siye, nilikumbana na mkasa mmoja ambao hakika ndio uliozaa mada yangu ya leo. Akina mama wawili, mtu na rafikiye, walikuwa wameketi siti moja wakizungumza kwa masikitiko makubwa.
Awali sikuelewa kisa ni nini, lakini baada ya muda mmojawao akapigiwa simu na baada ya kuzungumza na mtu huyo huku akipewa maelekezo, akasema kwamba wako njiani wanakwenda.
Alipokata simu mwenzake akamuuliza ni nani. Yule wa kwanza akasema kwamba wamempata mtu wanayemsaka. Mwenzake akamshauri awaambie waliompigia simu wampeleke huyo mtu polisi, lakini wakakubaliana kwamba haina haja kwa sababu walikuwa wamekaribia kufika. Wakateremka pale Keko Maflati karibu na uwanja wa taifa.
Hata hivyo, baada ya simu hiyo mmoja wao alikuwa akilaumu kwamba mtoto huyo wa kike amekuwa msumbufu sana. Ametafutiwa shule lakini badala ya kwenda huko akaamua kuzamia moja kwa moja anakokujua yeye.
“Akipelekwa polisi atasema tu alikokuwa na hao aliokuwa nao siku zote hizi. Yaani ni balaa kweli sisi wanawake, mtu wakati mwingine unaweza kusema bora uzae mwanamume hata akiwa jambazi atauawa huko potelea mbali kuliko mtoto wa kike ambaye daima anakupa presha,” akasema yule wa kwanza, ambaye nahisi ndiye mama mzazi wa binti huyo.
Hapo ndipo nilipoelewa kwamba kumbe walikuwa wakimsaka binti yao ambaye alitoweka nyumbani kwao siku kadhaa kwa maelezo kwamba yuko kwa rafiki zake anajisomea, kumbe siyo! Unaona mambo ya dunia haya ndugu zanguni?
Ni kwa mantiki hiyo basi leo nimeamua kuwaletea kibao hiki cha Rosa Nenda Shule, kibao kilichotungwa na Jabali la Muziki Tanzania, Marijani Rajab Marijani ‘Dozzer’, mwaka 1973 wakati huo akiwa na bendi ya Safari Trippers.
Matukio kama haya yametukuta wengi, tukiwa kama wazazi ama wanajamii. Watoto wa kike wanaosoma wanaleta matatizo sana, ingawa siwezi kuwatetea wale wa kiume nao kwani kila mmoja ana matatizo yake.
Na hapa lazima niseme kwamba, simuungi mkono yule mama anayesema bora mtoto wa kiume. Jamani mtoto ni mtoto tu, awe wa kiume au wa kike. Namna tabia yake itakavyokuwa ni malezi ayapatayo, ikiwa ni pamoja na kuepuka makundi na zaidi kumuomba Mungu amtangulie na ampe mwenendo mwema!
Hata hivyo, watoto wa kike wana matatizo makubwa sana kuliko wa kiume, hasa wanapoingia kwenye ule umri wa ujinga, yaani foolish age. Vichuchu vikianza kuchomoza tu na sauti nayo kubadilika, mtoto wa naye huanza kubadili tabia. Atachagua mavazi, vipodozi na hata mwendo ataubadilisha! Ndio umri wa balekhe huo ambao humfanya ajione kama yeye ndiye anayejua kila kitu.
Na hapa ndipo ninaposema kwamba, wengi wetu tumeshuhudia tabia za watoto hawa, wengine wakishindwa kumaliza masomo, na kama wanamaliza, basi huwa ni mbinde kweli kweli.
Tabia zao wengine hata walimu wao huziona jinsi zinavyobadilika na walimu wengine waungwana huwa wanapenda kuwasiliana na wazazi wa binti husika, kama Marijani anavyosema;
“Habari zako nimezipata kutoka kwa walimu wako, Kwamba siku nyingi zimepita na wewe shule mbona huonekani, Unaniaga baba nakwenda shule, Na mapesa mengi kuniomba, Kumbe muongo mkubwa ukitoka kumbe una njia zako...”
Hebu nielezni ndugu zangu, ni nani kati yetu ambaye hajashuhudia mambo haya? Mimi mwenyewe nimeshuhudia watu wengine wakishindwa kumaliza masomo na wale waliomaliza hufanya hivyo ili kutimiza wajibu.
Lakini hakuna mzazi ambaye hamtakii mema mwanawe, na ndiyo maana hivi sasa wazazi wote wako radhi kujinyima na hata kufanya vibarua ili kugharamia elimu ya watoto wao, kwa sababu ndio urithi wao.
Katu wasijidanganye kusema, “Aaah, baba yangu mimi tajiri, hata nisiposoma nitaishi tu!” Huu ni ujinga tena upumbavu. Hivi unajua mali aliyonayo babayo aliipata vipi? Unajua jinsi alivyosoma? Si walisema Waswahili kwamba nguo ya kuazima haistili maungo!
Tazama yule binti mwingine ninayemfahamu mimi ambaye baba yake alikuwa tayari kuachilia ujenzi wa nyumba ya familia ili amsomeshe baada ya kufaulu mtihani wa darasa la saba. Lakini alipokwenda shule akaingia kwenye makundi, akaanza kujirusha. Mtihani wa kidato cha pili ulipokuja, akaanguka vibaya sana, lakini nyumbani akadanganya kwamba amepasi. Siri ilipogundulika, akaamua kuachana na shule!
Marijani anasema hivi, hata mimi na mzazi mwingine anayewatakia maendeleo watoto tunasema hivi; “Ooo Rosa wewe nenda shule eeee, Ukimaliza faida utaiona eeee... Wacha tamaa Rosa ee wacha tamaa mama ee, Tamaa yako Rosa ee itakuponyesha… Ipende shule mama ee wacha uhuni mama ee.”
Labda nimalizie kwa kuwaasa hawa binti zetu kwamba, wanaume, yaani sisi wanaume, ashakum si matusi, ni washenzi kweli kweli. Wengi wao wanapenda kuwahadaa mabinti pale wanapoona wameanza kuchipukia. Wakishamaliza haja zao, na pengine tayari watakuwa wamewatwisha mimba, au hata magonjwa ya zinaa, haoo wanakimbia.
Utahangaika na mzigo wako peke yako na ndipo hapo huwa napenda kutumia ule msemo wa wahenga na wahenguzi kwamba, Kijuto msuto kisicho kito! Yaani Majuto ni mjukuu, upo hapo mama.
Hebu wadogo zangu ngoja niwaambie. Hayo mapenzi hayo mnayoyakimbilia yalikuwepo, yapo na yataendelea kuwepo. Walikuwepo akina babu na bibi, wameondoka wameyaacha. Sasa kwa nini msisubiri mkamaliza jambo moja na kasha muende jingine?
Halafu maskini ya Mungu, mara nyingi zaidi ukimfuatilia binti huyu utakuta huyo anayemzuzua ni mwanafunzi mwenzake ama muuza chips au hata kondakta wa daladala. Kama huyu mwanafunzi, ambaye dira yake haijui kabisa kwa sababu bado na yeye anahudumiwa na wazazi, halafu leo hii anakudanganya kwamba lazima akuoe! Hivi kwa nini muwe na akili za kuku kupewa mtama kwenye ungo na kisha kuumwaga na kuuchanganya na mchanga ndipo uudonoe?
Gonganisheni vichwa vyenu, halafu mtapata majibu sahihi, vinginevyo nendeni shule kwa sababu faida ni yenu wenyewe. Mali ya urithi ukiitegemea utakufa kibudu!
Wasalaaam!
Tazama mashairi ya wimbo wa Rosa:

[Wote]
Habari zako nimezipata kutoka kwa walimu wako
Kwamba siku nyingi zimepita na wewe Shule mbona huonekani
Unaniaga baba nakwenda Shule
Na mapesa mengi kuniomba

Kumbe muongo mkubwa ukitoka kumbe una njia zako

(repeat)

(Chorus)

[Wote]
Ooo Rosa wewe nenda shule eeee
Ukimaliza faida utaiona eeee......
Wacha tamaa Rosa ee wacha tamaa mama ee
Tamaa yako Rosa ee itakuponyesha

Ooo Rosa wewe nenda shule eeee
Ukimaliza faida utaiona eeee......
Ipende Shule mama ee wacha uhuni mama ee

Kwa majadiliano, hoja na ushauri gonga 0715 – 070109, au
brotherdanny5@gmail.com.

No comments:

Post a Comment