Thursday, 24 October 2013

KILIO CHA ASHURA NI CHA WANAWAKE WOTE!


Na DANIEL MBEGA

AHLANI Wasaalan wapendwa wasomaji wa blog hili. Ni matumaini yangu kwamba nyote mu' wazima popote pale mlipo na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku. Karibu kwa mara ya kwanza katika makala yetu hii ya kusawiri nyimbo mbalimbali zinazozungumzia maisha yetu ya kila siku.
Hapa tunazungumzia nyimbo mbalimbali za enzi zile, ambazo zinaonekana bado rasilimali kubwa katika sanaa ya muziki ambayo si vibaya hata tukaziita ni miongoni mwa rasilimali-kale.
Kwa kuwa nyimbo hizi zimeanza kusahaulika kwa vijana wa sasa, basi nimeona ni vyema tukumbushane wale vijana wa zamani zile kwa kuzichambua na kuelezea ujumbe maridhawa uliopo na nini tunachotakiwa kujifunza.
Siyo siri, nyimbo zile bado zina mguso wa aina yake na wale vijana wenzangu watakubaliana na mimi kwamba, ujumbe na mpangilio wake ulikuwa mzuri na kila mojawapo ya nyimbo hizo inaposikika redioni huwakumbusha hizo enzi, enzi ambazo si ajabu kumkuta shabiki wa Msondo Ngoma akicheza kifua wazi, shati kalifutika kwenye mfuko wa nyuma wa suruali na chupa kaiweka chini mbele yake. Ole wako kivuli chako kikatize kwenye eneo analochezea!
Hata hivyo, leo niko na kibao cha mwanzoni mwa miaka ya 1990 kinachokwenda kwa jina la 'Ashura' ambacho kiliimbwa na Nana Njige (sasa marehemu) wakati huo akiwa na bendi ya Magereza Jazz Band 'Wana Mkote Ngoma'.
Katika kibao hiki Nana Njige anasikika akilalama kwamba mumewe wa sasa anamfanyia visa visivyo kifani. Anasema; "...Visa ninavyofanyiwa na bwana huyu, Nimeamini methali isemwayo, Mkataa pema, pabaya panamwita... nilidanganyika, Kumuacha mume wangu, kumfuata bwana mwingine, Kumbe ni mwizi baba, kumbe ni muongo."
Ashura anazungumza wazi bila kificho, kwamba alidanganyika na kuamua kumwacha mumewe ili aende kwa mwanamume mwingine aliyemhadaa na mambo kadha wa kadha. Lakini matokeo yake mwanamume huyo ameonekana kuwa muongo, na zaidi mwizi.
Aaah, waliamba Waswahili; 'Kijuto msuto kisicho kito', wakiwa na maana kwamba majuto ni mjukuu. Nami nasema swadakta kabisa, kwa sababu huu ndio ujumbe halisi uliomo katika kibao hiki ambacho kilitingisha kweli kweli katika anga la muziki wa dansi nchini Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Kilichoonekana, na ambacho Ashura mwenyewe anakinadi ni kwamba, amejifunika shuka wakati tayari kumepambazuka! Laiti kama angalifikiria wakati bwana huyo anamrubuni, akatafakari kwamba kuisaliti ndoa yake ni kosa ambalo angekuja lijutia baadaye kama ajutavyo sasa, kamwe asingefikia hatua hiyo.
Lakini niseme wazi tu kwamba, akina Ashura wapo wengi mno katika jamii yetu. Wengi sana na idadi yao haina kipimo. Mambo yaliyompata Ashura yanawapata wanawake hawa kila kukicha na daima wanashindwa kujua wafanye nini ili kuyarejesha mapenzi yaliyopotea.
Niseme wazi tu kwamba, wanaume, ashakum si matusi, ni washenzi, tena washenzi kweli kweli. Wapo wengi wao ambao wanapenda kuwanyatia wake za watu tu, au niseme, wanawake ambao tayari wako kwenye uhusiano.
Wao huwa wanasema kwamba wanawake hao hawana gharama kubwa kwa sababu hawawezi kuwasumbua kwa kodi ya nyumba wala pesa ya chakula. Si wameolewa na waume zao, kodi ya nini tena? Au pesa ya chakula ya nini wakati kila siku bwana wake anamwachia pesa ya matumizi!
Wanafahamu kwamba mwanamke aliyeolewa hataweza kuwadai fedha za nguo kwa sababu si itakuwa balaa kwa waume zao? Unadhani watasemaje pindi watakapokuwa wameonekana na nguo mpya za gharama wakati uwezo wa waume zao ni mdogo?
Hii ndiyo faida ambayo wanaume hawa wakware huwa wanaiona na gharama pekee ambayo wanaweza kuingia kwa hawa wake za watu ni matumizi madogo madogo tu kama chips-kuku, vipodozi na kadhalika, vitu vidogo ambavyo si ajabu mwanamke akamdanganya mumewe kwamba amenunua baada ya kupokea fedha zake za mchezo. Si mnafahamu kwamba michezo ya kupeana imeenea hata maofisini?
Ashura mwenyewe anasema hivi; "...Muheshimu ndoa zenu zisijevunjika, Muachane na mabwana wadanganyifu eeeh, Atakupenda wakati una mumeo ooh, Ukishaachika wala hana habari nawe, Atakudanganya kwa curl na relaxer, ... Na starehe za muda hazina mwisho sikia..."
Lakini pia wapo wanawake ambao baada ya kufuatwa na wanaume hawa, wakigeuka nyuma kuona kwamba wana matatizo katika ndoa zao, hukurupuka na kuwaendea hao wadanganyifu baada ya kuhadaiwa kwa vitu vidogo vidogo ambavyo vimekuwa adimu kwa waume zao.
Ndiyo. Hili si jambo la ajabu. Mnapokuwa kwenye ndoa, mara nyingi kutokana majukumu ya kifamilia ambayo huwa yanazidi hasa pale watoto wanapokuwa wamezaliwa, baadhi ya vionjo vya ndoa kama mabusu, maneno matamu ya 'mpenzi', 'laazizi' na kadhalika huwa yanapungua.
Lakini yanapungua tu si kwamba mwenzako hakupendi, bali kutokana na majukumu na kujisahau, jambo ambalo ni dogo ikiwa tu mtatafuta muda wa kutafakari na kujirekebisha katika jitihada za kuboresha mapenzi yenu badala ya kukimbilia kwa mwanamume mwingine kwa vile tu analitamka neno 'nakupenda' zaidi ya mara elfu moja.
Kumbuka kwamba, kwenda nje ya ndoa siyo suluhu ya matatizo, iwe kwa mwanamke ama mwanamume, bali kutazidisha matatizo ikiwa hata kuachana na mmoja wenu akishakumbuka kwamba pembeni kuna mtu ambaye kila wakati anamsumbua kwa kumwambia anampenda, basi kiburi kitaibuka nyumbani na kuzaa tamaa.
Tunaambiwa kwamba tamaa ikipata mimba huzaa dhambi na hakuna dhambi mbaya zaidi kama zinaa, kwani tunaambiwa haisameheki kwa vile inafanyika kwenye mwili ambalo ni Hekalu la Mungu.
Suluhu la matatizo yoyote ndani ya familia na hasa ndoa, ni majadiliano. Tafuteni muda wa kutosha kuwa pamoja na kuzungumza mambo mbalimbali ili kudumisha ukaribu, kwa sababu kutokufanya hivi hujenga daraja baina yenu na inakuwa rahisi kwa mmoja wenu kushawishika kwenda nje ya ndoa.
Lakini pamoja na hayo, lazima muwe na kumbukumbu kwamba nyote wawili mmekula yamini ya kuishi pamoja milele; kwa shida na raha, hadi kifo kitakapowatenganisha. Iweje leo Brother Danny baada ya kufilisika umuone si lolote si chochote na kuamua kukimbilia kwa Saidi? Au inakuwaje baada ya mkeo Zuhura, ambaye ulimpenda wakati ule kutokana na umbile lake jembamba, awe hana thamani leo hii baada ya kuzaa watoto na kuwa mnene? Zi wapi basi hizo ahadi zenu? Lazima tubadilike wanajamii kama kweli tunataka kujenga heshima zetu katika ndoa.
Kabla ya kuwaaga, nawaletea mashairi yote ya kibao cha Ashura, lakini msikose kuwa nami katika blog hii kila sikuili tukumbushane mashairi ya vigongo vya zamani. Kwa herini. Sikiliza mashairi ya Ashura:


Ashura mimi najuta, Mwenzenu kweli najuta sasa x2

Visa ninavyofanyiwa na bwana huyu [Bwana huyu]
Nimeamini methali isemwayo [isemwayo]
Mkataa pema, Oooh, pabaya panamwita x2

Leo hii mwenzenu, Kusema hivi mimi, Nina maana yangu, nilidanganyika,
Kumuacha mume wangu, kumfuata bwana mwingine,
Kumbe ni mwizi baba, kumbe ni muongo.

Visa ninavyofanyiwa na bwana huyu [Bwana huyu]
Nimeamini methali isemwayo [isemwayo]
Mkataa pema, Oooh, pabaya panamwita x2


Kibwagizo:
Nawausia wanawake wenzangu wote eeh, Muheshimu ndoa zenu zisijevunjika x2

Muachane na mabwana wadanganyifu eeeh, Atakupenda wakati una mumeo ooh,
Ukishaachika wala hana habari nawe [Hana habari nawe]

Atakudanganya kwa curl na relaxer, Atakudanganya kwa khanga za Mombasa,
Atakudanganya kwa vitenge vya Zaire, Atakudanganya kwa chips na mayai,
Na starehe za muda hazina mwisho sikia

Nawausia wanawake wenzangu wote eeh, Muheshimu ndoa zenu zisijevunjika x2


<MWISHO>.


Mnaweza kunitumia mchango wenu kwa sms ama kunipigia kupitia kilongalonga – +255 715 – 070 109, au barua-pepe: brotherdanny5@gmail.com.

No comments:

Post a Comment