L'Okanga La Ndju Pene Luambo Luanzo Makiadi 'Franco'
Na Daniel
Mbega
HAPAN’SHAKA
yoyote kwamba mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku vyema kabisa huko mliko.
Leo nawaletea kibao cha Lisolo ya Adamo
na Nzambe, yaani ‘Mazungumzo ya Adam
na Mungu’, upo hapo mwanakwetu?
Basi
mwanangu, kibao hiki kiliimbwa na L’Okanga La Ndju Pene Luambo Luanzo Makiadi,
ukipenda unaweza kumwita Francis Makiadi, au Franco, mzaliwa wa Sona Bata
katika Jimbo la Bas Congo nchini DRC mnamo Julai 6, 1938, ambaye hata hivyo
alifariki dunia mjini Brussels, Ubelgiji Oktoba 12, 1989.
Jamaa
huyu ndiye mtu pekee aliyeitangaza sana Afrika kupitia muziki na akawafanya
Wazungu waukubali muziki wa Kiafrika badala ya kuendelea na kasumba yao ya
kuziita tamaduni zetu eti za kishenzi!
Hata
hivyo, leo nimeuchomoa wimbo huu wa Lisolo
ya Adamo na Nzambe (yaani Mazungumzo ya Adam na Mungu) kwenye albamu yake
iitwayo OK Jazz Volume 3, iliyotolewa
katika ‘lebo’ ya African Sonodisc mwaka 1977, ambayo pia ilikuwa na nyimbo
nyingine kama Mbongo, Lotambe, Badjekate,
Tambwe Lutandila na Moleka Okoniokolo
Ngai Ntina.
Basi
katika kibao hiki Franco, ambaye pia ameshiriki kupiga gitaa la solo,
ameshirikiana na akina Mavatiku Visi maarufu kama Michelino aliyekuwa akipiga
gitaa la solo, Lutumba Massiya Simaro, Josky Kiambukuta Londa, na wengineo
wengi waliokuwa wakiunda kundi zima la Tout Puisant Orchestre Kinnie – yaani TP
OK Jazz, unanipata lakini? Tozali moko baninga na bandeko na ngai?
Wimbo huu
umeimbwa Kilingala, lakini mimi nimeutafsiri wote ili uweze kuupata ujumbe
wake. Kama unataka kuusikiliza, tafuta CD, kaseti au LP.
Yanayosemwa
na Franco ni mambo ya kweli kabisa yanayotokea katika maisha ya kila siku ya
mwanadamu. Anazungumzia namna binadaamu alivyogeuka na kumwacha Mungu, na sasa
anafanya mambo ya ajabu yanayomkasirisha muumba.
Yeye
anaanza kwa kusema; “Eva aliumbwa kutoka
ubavuni mwa Adam, Adam aliliona jua kabla yake, Adam alizungumza na Mungu kabla
yake, Alizungumza pia kuhusu shetani? Lakini Biblia… Sikumbuki mlango wa ngapi,
Imekuwaje mwanamke awe shetani anayewaangamiza wanaume? Nani aliyetufundisha
ushetani huu? Utasema Eva alikuwa wa kwanza kula tunda haramu, Nani alimpa Eva
tunda hilo? Ulijifunza kwamba Malaika wa kike, Aligombana na Mungu, Ili
akuumize wewe? Wanaume, ninyi ndio matatizo yenu na wanaume wenzenu…”
Umeyasikia
sana hayo ndugu yangu? Basi ndivyo Franco anavyoanza kueleza. Ni kweli kabisa,
wanaume ndiyo chanzo cha matatizo, hata kama tutawalaumu wanawake. Mwanamume
ndiye anayeanza kumchokoza mwanamke, lakini ni nadra sana kumkuta mwanamke
anamtongoza mwanamume, hasa kwa mila zetu za Kiafrika, na kama itatokea hivyo
unaweza kusema kwamba mwanamke huyo ana kasoro au malaya! Siyo kweli hata hivyo
kwa sababu sote tunazo hisia za kutamani, kupenda na hata kuchukia.
Lakini
ushetani wa wanaume uko dhahiri, kama unabisha hebu sikiliza hapa; “Unamtazama mke wa jirani yako, Unataka
kumtongoza, Unamtazama binti ya jirani yako, Unaanza kummendea, Mkeo anapoanza
kutongozwa, Unakimbilia kwa majiji, Unataka wapatikane na hatia.”
Sasa
ndugu yangu umesikia hivyo? Mambo haya hayatokei kwenye jamii zetu jamani? Ni
wangapi walioripotiwa na magazeti kwamba wamefumaniwa, ama na wake za watu au
vibinti vya watu? Jiulize, wanawake hao, ama mabinti hao, ndio waliowatongoza
wanaume hao?
Utakuta
wanaume wengine hata soni hawana. Kusaidiana ni jambo la kawaida katika jamii,
lakini akiombwa msaada na mke wa jirani yake, au hata binti wa jirani yake,
basi yeye anataka alipwe fadhila, na si fadhila nyingine zaidi ya ngono!
Franco
anasema; “Ukimuona mke wa jirani yako
mwache aende…mwache aende, Ukimuona mtoto wa jirani yako mwache aende …mwache
aende, kumbuka kwamba wewe pia una mke na watoto, Kumbuka kwamba hili ni tatizo
la rafiki yako pia.”
Swadakta
kabisa. Hiyo ndiyo kuntu nturuba haswa. Yale unayoyafanya na wenzako
wanafanyiwa ama wanayafanya. Matatizo kama hayo yatakukuta na wewe pia, kwa
maana nyingine, ni matatizo ya jamii nzima na mtu mwenye kuyakomesha ni wewe na
mimi.
Watu
wengine hawana huruma hata kidogo. Wako tayari kuwanyanyasa jirani zao bila
aibu, kwa kuwa tu wao wamebahatika kuwa na hali fulani. Kwa kutumia uwezo
alionao, anataka afanye ufirauni kadiri apendavyo.
“Mtoto wa jirani yako, Aliyeumbwa mamchoni
pako, Mtoto wa jirani yako, Aliyekua machoni pako, Kwa kuw amatiti yake
yamekua, Unamtamani na kutaka kumuoa, Huna aibu?”
Wanadamu
wengine bwana, eti wakishapata mali wanataka kujibadili kama kinyonga. Wanataka
wawapate wanawake wote wazuri. Wanaanza kuwadharau hata wanawake wao, ambao
wamepigana pamoja mpaka kuweza kupata mali hizo.
“Wakati ulipokuwa maskini, Ulioa mwanamke
mbaya, Kwa kuwa sasa ni tajiri, Unaanza kutamani wanawake warembo, Kwanza
mfukuze mwanamke mbaya, ndipo uoe mwanamke mrembo… Leo unamiliki Mercedes,
Unasema unataka mwanamke anayezungumza Kifaransa, Mke wako, wakati ulipomuoa,
Hukujua kwamba unaweza kuwa tajiri siku moja, Tazama mambo yanavyoweza kutokea,
Hatutaki hivyo..”
Lakini
kwa kuwa watu hawa tunao katika jamii zetu, tunapaswa kuwaambia ukweli; “Acha unafiki wako wa kizamani,
Tunakufaahamu, Mheshimu mke wa jirani yako, Acha kuwa mnafiki, Rafiki zako
wanakujua, Acha kukataa… Waache wake za wale unaofanya nao kazi kampuni moja,
Wote wanafahamu kwamba wewe unawatamani wake zao, Lakini waache, waache, Acha
wake za rafiki zako…
“Kwako wewe, wanawake wazuri wanaweza
kununuliwa kwa fedha, Rafiki zako wameoa wanawake wazuri, Wakati walipokuwa
katika hali nzuri, Leo unadhani unaweza kuwaumiza watu, Kwa kuwa una fedha…
Haya macho yako, unatamani wake wa wenzako, Yatang’olewa siku moja, Haya macho
yako, unatamani binti za wenzako, Yatang’olewa siku moja, Jihadhari na wanawake
wa wenzako, Jihadhari na binti za wenzako, Unajitafutia matatizo…”
Mwasikia
sana bandugu? Kibao hiki ni kitamu sana kinachezeka katika ule mtindo wa
rhumba, miziki ya bakulutu, lakini ujumbe uliomo ni mzito na unatakiwa kuzama.
Shairi ni
refu sana na nimelazimika kunyofoa baadhi ya beti. Si mnamfahamu mzee mzima
jinsi alivyokuwa akitunga nyimbo ndefu? Muziki ukipigwa unaweza kusinzia,
ukiamka unakuta muziki unaendelea.
Tukutane
tena wakati mwingine!
Mnaweza
kunitumia mchango wenu kwa sms ama kunipigia kupitia kilongalonga – 0715 – 070
109, au barua-pepe: brotherdanny5@gmail.com.
No comments:
Post a Comment